1. Maana ya Elimu Jumuishi
Elimu jumuishi ni mfumo wa elimu unaotoa fursa kwa watu wote kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kujifunza bila kujali tofauti zao za kimaumbile, kihali, kiakili, kijinsia au kikabila. Mfumo huu unalenga kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayebaguliwa, hasa wale wenye mahitaji maalumu.
2. Lengo Kuu
Kuwezesha kila mtu kupata elimu stahiki kulingana na mahitaji yake binafsi.
Kuondoa vikwazo vinavyozuia ushiriki wa wanafunzi katika elimu.
Kukuza usawa na ujumuishaji katika mazingira ya kujifunza.
DARASA JUMUISHI
Darasa jumuishi ni mazingira ya kujifunzia ambapo mwalimu na wanafunzi hushirikiana kwa karibu. Mwanafunzi hujihisi salama, anahimizwa kutoa maoni na kushiriki kikamilifu katika shughuli za darasa. Wanafunzi katika darasa hili huwa na mahitaji na changamoto tofauti za ujifunzaji, hivyo ni muhimu mwalimu kufahamu idadi yao, tabia na mitindo ya ujifunzaji ili kutoa afua stahiki.
SIFA ZA ELIMU JUMUISHI
Usawa na Ujumuishaji Elimu jumuishi huondoa ubaguzi wowote kwa kuhakikisha kila mwanafunzi anashiriki kikamilifu katika mchakato wa kujifunza bila kuathiriwa na hali yake ya kimwili, kiakili au kijamii.
Kutambua Mahitaji Tofauti ya Wanafunzi Mfumo huu hutambua na kuheshimu tofauti za wanafunzi, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kiakili, hali ya kimwili, kijinsia na asili ya kitamaduni.
Utoaji wa Huduma Maalum Elimu jumuishi hutoa huduma maalum kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili kuhakikisha wanashiriki kikamilifu na kufanikiwa katika ujifunzaji.
Ushirikiano na Mawasiliano ya Karibu Mafanikio ya elimu jumuishi hutegemea ushirikiano kati ya walimu, wazazi na wataalamu kama vile wanasaikolojia. Mawasiliano haya husaidia kutambua mahitaji ya mwanafunzi na kuweka mikakati ya kumsaidia.
Mazingira Rafiki na Wezeshi Mazingira ya kujifunzia yanapaswa kuwa salama, yenye vifaa vinavyofikika kwa urahisi na yanayowezesha ushiriki wa wanafunzi wote bila vikwazo.
Mbinu Bunifu za Ufundishaji Elimu jumuishi hutumia mbinu za ufundishaji zinazozingatia mahitaji ya kila mwanafunzi, ikiwa ni pamoja na mbinu shirikishi, za vitendo na zinazompa mwanafunzi nafasi ya kujieleza.
UMUHIMU WA ELIMU JUMUISHI
Kujenga Maarifa na Ujuzi kwa Wote Elimu jumuishi huwasaidia wanafunzi wote, wakiwemo wenye mahitaji maalumu, kupata maarifa na ujuzi unaowawezesha kushiriki kikamilifu katika jamii.
Kukuza Mshikamano na Uvumilivu Kwa kujifunza pamoja, wanafunzi hujenga uwezo wa kuelewana, kuheshimiana na kuthamini utofauti wao, jambo linalochangia kujenga jamii yenye mshikamano.
Kuwezesha Kujitegemea kwa Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalumu Kupitia elimu jumuishi, wanafunzi wenye mahitaji maalumu hujifunza stadi za maisha zinazowawezesha kujitegemea na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Kuhakikisha Haki ya Msingi ya Elimu kwa Kila Mtu Mfumo huu unazingatia haki ya kila mwanafunzi kupata elimu bila kujali hali yake ya kimwili, kiakili au kijamii.
Kutoa Afua Stahiki na Mpango Binafsi wa Ujifunzaji Elimu jumuishi huweka mikakati maalum kwa kila mwanafunzi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vifaa saidizi na zana za kujifunzia ili kumwezesha kufikia uwezo wake wa juu.

